Wanaharakati Vijana 30 Wazindua Mpango wa Usawa wa Kijinsia Afrika Mashariki
28 Oktoba 2024 l Women Deliver leo inatangaza wanaharakati vijana 30 ambao wanaongoza utetezi wa suala la usawa wa kijinsia katika Afrika Mashariki kama kundi la kwanza la Mpango wake wa Viongozi Chipukizi kwa Ajili ya Mabadiliko.
Hii ni programu ya kimkakati ya miaka miwili inayowapa vijana watetezi ufadhili, rasilimali, mafunzo, na ufikiaji kwa watoa maamuzi, inayolenga kukuza juhudi zao za utetezi unaozingatia vijana katika nafasi za kitaifa, kikanda, na kimataifa ili kuendeleza uhuru wa kimwili wa wasichana waliobalehe. Women Deliver itazindua programu katika maeneo mengine kila mwaka kwa mfululizo.
“Kwa kuungana, vijana wanaweza kuunda sauti yenye nguvu ya pamoja na kupigania mabadiliko ya sera, hali itakayoendeleza mshikamano wa kimataifa,” anasema Clara Benjamin (24) ambaye ni mwanachama wa kikundi kutoka Tanzania.
Kundi la kwanza la Mpango wa Viongozi Chipukizi linajumuisha wanaharakati, wenye umri wa miaka 15 hadi 29, kutoka Burundi, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda. Kundi la Afrika Mashariki litaanza Oktoba 2024 hadi Septemba 2026.
“Sasa ni wakati wa vijana kuelekeza shauku na kujitolea kwao katika kutetea ulimwengu bora ambapo mahitaji na matarajio yao yanatambuliwa na kushughulikiwa,” asema mwanachama wa kikundi Eden Alem (28), kutoka Ethiopia.
Ikiwa na watu milioni 116.8 walio na umri wa chini ya miaka 35, Afrika Mashariki ni eneo lililojaa uwezekano wa ushiriki wa vijana katika nafasi za utoaji maamuzi. Hata hivyo, kutokana na kuongezeka kwa pingamizi za kupinga haki – hasa kwa maeneo ambayo yanaathiri wasichana waliobalehe, wanawake, na watu wa jinsia tofauti – hitaji la utetezi unaozingatia vijana bado ni muhimu. Pamoja na changamoto hizi, mzozo unaohusu tabianchi unaendelea kulemea bara hili, huku ukame mkali katika miaka ya hivi karibuni ukiathiri mamilioni ya watu.
Women Deliver inaamini kuwa Mpango wa Viongozi Chipukizi utasaidia kuimarisha ushirikiano na mshikamano na vijana katika kanda, wanapoendelea kuendeleza malengo yao ya utetezi kwa mustakabali sawa na endelevu katika jamii zao.
“Ni muhimu kuungana kwa sababu tutaweza kubadilisha hadithi za watoto wengine na vizazi vijavyo,” asema mwanachama wa kikundi Miriam Mwau (15), kutoka Kenya.
Maswali ya vyombo vya habari: Kim Lufkin, Mkurugenzi wa Mawasiliano, media@womendeliver.org
Kuhusu Women Deliver:
Women Deliver ni shirika la kimataifa la utetezi linaloongozwa na lengo moja: kwamba kila msichana na mwanamke afurahie haki zake za uhuru kamili wa kimwili na kiafya. Jifunze zaidi: www.womendeliver.org.